Sunday 22 June 2014

TATIZO LA KUOTA MATITI KWA WANAUME NA WATOTO (GYNECOMASTIA)


            Picha ya mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 13
Tatizo la kuota matiti kwa wanaume na watoto limekuwa kubwa sana katika dunia ya leo. Inawezekana kabisa wakati unatembea njiani ukaona wanaume au watoto wadogo wa kiume wakiwa na matiti makubwa ambapo watu wengi huchukulia kama ni kawaida. Kitaalamu gynecomastia ni kukuwa kuliko kawaida yake kwa tishu ya kwenye titi inayojulikana kama glandular tissue. Tatizo hili huonekana sana kwa watoto wachanga na wanaume waliokatika umri wa kubaleghe, lakini pia huonekana kwa watu wazima na wazee.

Ukubwa wa tatizo (epidemiology)
Asilimia 60-90 ya watoto wachanga wanapata tatizo hili la kukuwa kwa matiti kwa mpito linalojulikana kitaalamu kama transient gynecomastia kutokana na kuwepo kwa kichocheo cha aina ya estrogen kwa wingi wakati wa ujauzito wa mama.
Kati ya asilimia 4-69 ya vijana walio katika umri wa kubaleghe imeonekana wanapata tatizo hili kutokana na kuwepo kwa wingi kwa kimengenyo aina ya estradiol.Mara nyingi huonekana katika umri kati ya miaka 10-12 na hupotea taratibu ndani ya miezi 18, si kawaida yake kuonekana kwa vijana walio na umri ya zaidi ya miaka 17. Asilimia 24-65 ya watu wazima hupatwa na tatizo hili, hii hutokana na kubadilishwa kwa wingi kwa kichocheo aina ya testerone kuwa estradiol na kutolewa kwa uchache kwa kichocheo hiki cha testerone kutoka kwenye korodani zinazoanza kuzeeka..Ikumbukwe ya kwamba kichocheo hiki testerone hutengenezwa katika korodani za mwanamume.

Pathofiziolojia (Nini hutokea?)
Kuongezeka ukubwa wa matiti kwa wanaume hutokana na kuharibika kwa mfumo wa vichocheo unaojulikana kama estrogen-androgen balance na hivyo kusababisha estrogen kutolewa kwa wingi ama kuongezeka kwa msisimko (sensitivity) wa matiti kwa kiwango cha zaidi ya kawaida kwa kichocheo aina ya estrogen kilicho kwenye mzunguko wa damu.Estrogen husababisha chembechembe zinazojulikana kama ductal epithelia kuongezeka kwa wingi, kurefuka (ductal elongation) na kugawanyika, kuongezeka kwa chembechembe za mafuta (ductal fibroblasts) na kuongezeka kwa mfumo wa damu kwenye matiti (increase vascularity).Estrogen hutengenezwa kutoka kwenye vichocheo vya testerone na androgen kwa kutumia kimengenyo kinachojulikana kama aromatase.

Aina za gynecomastia
•Puffy nipples – Kuongezeka ukubwa wa chuchu za matiti kutokana na kuongezeka kwa tishu aina ya glandular tissue.
•Pure glandular gynecomastia – Huonekana sana kwa wale wanaofanya mazoezi ya kujenga mwili (bodybuilders), kutokana na matumizi ya dawa za kujenga mwili (anabolic steroids) ambazo zinakuwa na kiwango kikubwa cha kichocheo aina ya testerone, ambacho hubadilishwa kuwa estrogen. Kwa wanaume wembamba, tatizo hili hutokea kutokana na kuongezeka kwa breast tissue gland pamoja na kuwepo/kutokuwepo kwa tishu aina ya adipose tissue.

Ni nani aliyekatika hatari ya kupata tatizo hili?
•Wanaume walio na umri zaidi ya miaka 50.
•Wenye uzito uliopitiliza (Obesity)
•Unywaji pombe kupindukia
•Magonjwa sugu ya figo au ya Ini
•Kuwepo kwa historia ya tatizo hili katika familia.

Visababishi vya kukuwa kwa matiti kwa wanaume
•Pseudogynecomastia – Kuongezeka kwa tishu zinazozunguka chuchu za matiti na huambatana na kuwepo kwa wingi wa tishu aina ya adipose. Mazoezi na kula vyakula venye virutubisho sahihi huondosha tatizo hili.
•Unilateral/asymetrical gynecomastia – Ni kuongezeka kwa titi moja pekee au la upande mmoja wa mwili wa mwanamume kutokana na sababu mbalimbali. Titi la upande wa pili huwa kwenye umbile na saizi ya kawaida. Bilateral gynecomastia ni kuongezeka kwa matiti yote mawili.

•Hypogonadism – Kutofanya kazi kwa korodani vizuri na kuwa ndogo. Hii husababishwa na magonjwa mbalimbali kama klinifelter'rs syndrome, pitituary insuffiency na nk.

•Umri – Kuzeeka pia kumehusishwa kutokea kwa tatizo hili kutokana na kutolewa kwa uchache kwa kichocheo cha testerone na kuongezeka kwa juhudi za kutengeneza kwa wingi kwa kimengenyo aina ya estradiol kutoka kwenye kichocheo aina ya testerone. Pia mabadiliko ya mfumo mzima wa vichocheo mwilini hasa kwa wale wenye uzito uliopitiliza.

•Uzito uliopitiliza (Obesity) – Watu wenye uzito uliopitiliza hupatwa na tatizo hili kutokana na kuharibika kwa mfumo wa vichocheo mwilini na hivyo kuongezeka kwa kichocheo aina ya estrogen mwilini mwao na wakati huohuo kupungua kwa kichocheo kingine aina ya testerone.

•Saratani – Baadhi ya saratani kama saratani ya kwenye korodani, kwenye tezi lililojuu ya figo (adrenal gland), saratani ya tezi la kichwa (pitituary tumor), huharibu mfumo mzima wa vichocheo mwilini hasa wa kuweka sawa vichocheo kati ya uanaume na uanawake (male-female hormonal balance).

•Hyperthyroidism – Kukuwa kwa ukubwa wa tezi la koo (thyroid gland) na hivyo kutengeneza kwa wingi kichocheo aina ya thyroxine.

• Tatizo la figo kushindwa kufanya kazi (Renal/Kidney failure) - Nusu ya wagonjwa wote wanaotibiwa tatizo la figo kushindwa kufanya kazi kwa kutumia hemodialysis hupatwa na tatizo hili la kukuwa kwa matiti kutokana na kuharibika kwa mfumo wa vichocheo mwilini (hormonal imbalance).

•Matatizo ya Ini – Dawa za kutibu magonjwa ya kwenye Ini kama liver cirrhosis, liver failure husababisha kutokea kwa tatizo hili kutokana na kukosekana kwa uwiano sawa wa mfumo wa vichocheo mwilini.

•Utapia mlo, ukame – Utapia mlo, ukame au kujikondesha husababisha kupungua kwa kichocheo aina ya testerone na kuongezeka kwa kichocheo aina ya estrogen na hivyo kuharibu mfumo wa vichocheo mwilini. Hii hutokana na 

kukosekana kwa virutubisho sahihi mwilini ambavyo vingi husaidia kurekebisha mfumo wa vichocheo mwilini na hivyo kumuepusha mtu na magonjwa mbalimbali pamoja na tatizo hili.
•Madhara ya dawa za kurefusha maisha (Antiretroviral therapy) kwa wagonjwa wa ukimwi.
•Utumiaji wa madawa ya kulevya kama bangi/marijuana.

Vipimo vya Uchunguzi
Vipimo hivi vitafanywa kulingana na historia ya mgonjwa, dalili na viashiria vya mgonjwa baada ya kupimwa na daktari.

•Kipimo cha damu (Complete Blood Count) – Kuangalia wingi wake, aina mbalimbali za chembechembe za damu na uwepo wa maambukizi ya bakteria.

•X-ray ya matiti (Mammogram) – Hutumiwa kuangalia tishu za kawaida na zile ambazo si za kawaida zilizo kwenye matiti. Husaidia kugundua uwepo wa saratani, cysts, na calcifications kwenye matiti.

•Liver function test – Mjumuiko wa vipimo vya damu kuangalia aina mbalimbali za vichocheo na vimengenyo ili kuweza kutambua kama mgonjwa ana ugonjwa wowote ule wa Ini na chanzo chake, vipimo hivi huangalia albumin, Alanine transaminase (ALT), Aspartate transaminase (AST), Alkaline phosphatase (ALK), Total bilirubin (TBIL), Direct bilirubin (Conjugated Bilirubin), Gamma Glutamyl Transpeptidase (GGT), Lactate Dihydrogenase (LDH).

•Tumor markers – Kipimo cha damu cha kuangalia viashiria vya saratani ya korodani kama AFP alpha feto 1 protein, Beta-HCG, LDH.

•Kipimo cha damu cha kuangalia wingi wa kichocheo cha aina ya testerone (Total and Free Testerone) Hufanyika asubuhi ambapo kiwango cha testerone huwa juu. Kiwango cha kawaida cha kichocheo cha testerone ni 300 - 1000 ng/dl (Kiwango hiki hupungua kwa asilimia 13 wakati wa mchana).

•Kipimo cha damu cha kuangalia vichocheo vinavyoonekana kwenye ugonjwa wa kukua ukubwa wa tezi la koo ( hyperthyroidism) kama kichocheo aina ya Thyroid Stimulating Hormone (TSH) ambacho huwa katika kiwango kidogo 

wakati wa kuugua ugonjwa wa hyperthyroidism, hutolewa na tezi la kwenye kichwa aina ya pitituary gland, vichocheo vyengine aina ya anti-TSH receptor antibodies (kwa wenye ugonjwa wa Grave’s disease), anti-thyroid – peroxidase 

(kwa wenye ugonjwa wa Hashimoto’s disease), na pia kuangalia wingi wa vichocheo aina ya T3 na T4. Kipimo cha Thyroid Scintigraphy pia huweza kutumiwa kutofautisha kati ya ugonjwa wa hyperthyroidism na ugonjwa wa thyroiditis. Kipimo hiki hutumia madini ya mionzi ya iodine (Iodine-131 ama Iodine-123).

•Vipimo vya kuangalia kama figo zimeshindwa kufanya kazi vizuri kama;

a)Kipimo cha utendaji kazi wa figo (Renal function tests) ambacho husaidia kuchunguza kiwango cha urea (blood urea nitrogen (BUN) katika damu. Aidha husaidia pia kuchunguza ongezeko la kiwango cha creatinine katika damu.

b)Uchunguzi wa kiwango cha madini mbalimbali katika damu (blood electrolytes)

c)Kupima kiasi cha mkojo kinachotolewa na mgonjwa katika masaa 24

d)Uchunguzi wa mkojo (Urine analysis): Rangi ya mkojo, kiasi cha electrolytes, uwepo wa usaha au damu au casts.

e)Ultrasound ya figo na kibofu cha mkojo

f)Renal biopsy.

Tiba ya Gynecomastia
Kama nilivyosema hapo awali, tatizo hili kwa vijana waliokatika umri mdogo au wa kubaleghe hupotea lenyewe taratibu ndani ya miezi 18. Kwa mzazi unatakiwa usihofu, lakini kama litaonekana kwa mtoto zaidi ya miaka 17, basi hapa mzazi unatakiwa kuchukua hatua za haraka ambazo ni kumuona daktari ili aweze kukusaidia kwa ufasaha zaidi.

1.Tiba ya madawa
•Tiba ya kutumia vichocheo (Testerone Replacement Therapy) – Kichocheo aina ya testerone hutolewa kwa mgonjwa kwa njia ya mdomoni, kwenye dripu, au kipachiko (patch forms). Hii hutolewa kwa wagonjwa ambao hawawezi 

kutoa testerone kutoka kwenye korodani zao kutokana na kupata ajali, ugonjwa au wale ambao hawana korodani kutokana na sababu mbalimbali.

•Dawa aina ya Selective Estrogen Receptor Modulator (SERMs) kama Tamoxifen, raloxifen, husaidia kupunguza ukubwa (volume) wa matiti lakini haziondoi tishu zote kwa ujumla. Aina hii ya tiba hutumiwa kwa wale wenye 

tatizo sugu la gynecomastia au wale wenye kupata maumivu makali sana. Dawa hizi zina madhara na hivyo ni vizuri kutumia kwa maelekezo ya daktari.

•Dawa aina ya Aromatase Inhibitors kama anastrozole, hufanya kazi kwa kuzuia kimengenyo aina ya aromatase na hivyo kuzuia utengenezwaji wa kichocheo aina ya estrogen. Tafiti nyingi zilizofanywa zimeshindwa kutoa majibu ya 

uhakika juu ya matumizi ya dawa hizi katika kutibu tatizo hili la kukuwa kwa matiti kwa wanaume.

2.Tiba ya Upasuaji – Kwa wale wenye tatizo hili sugu, upasuaji wa kurekebisha matiti unaweza kufanyika. Hii humuongezea mwanamume hali ya kujiamini na hivyo kuwa katika hali nzuri kisaikolojia, na huongeza ufanisi wa maisha yake ya kila siku.

3.Kupunguza uzito kwa kufanya mazoezi mara kwa mara na kula mlo wenye virutubisho vyote muhimu.

4.Kutibu chanzo au magonjwa mbalimbali kama hyperthyroidism, ugonjwa wa figo kushindwa kufanya kazi, saratani mbalimbali na nk.

5.Kuacha kunywa pombe na matumizi ya madawa ya kulevya kama bangi/marijuana.

6.Daktari kumbadilishia mgonjwa dawa baada ya kuona dalili za tatizo hili kwa wale wenye kutumia dawa za kutibu ugonjwa wa Ini, dawa za kurefusha maisha. Kwa wagonjwa wa Ukimwi, ni vizuri kwa daktari kabla ya kumpa 

mgonjwa dawa, kumfanyia mgonjwa kipimo cha fasting lipid profile, ili uweze kutambua kama dawa unazotaka kumpa zitamletea madhara au la. Na 

inashauriwa kurudia kipimo hiki kati ya miezi 3 hadi 6 baada ya kuanza dawa hizi za kurefusha maisha au baada ya kumbadilishia mgonjwa dawa. Hata hivyo sio dawa zote za kurefusha maisha zilizo na madhara haya, kwani zipo nyingine zinazopunguza kiwango cha mafuta mwilini na kwenye tishu.

Madhara ya Gynecomastia
1.Uwepo wa tatizo hili kwa muda wa zaidi ya miezi 12 au mwaka mmoja, husababisha matiti kutengeneza makovu au kwa kitaalamu scarring/fibrosis na hivyo kufanya tiba kwa kutumia dawa kuwa ngumu sana.

2.Wanaume wenye tatizo hili wapo kwenye hatari zaidi ya mara tano ya kupata saratani ya matiti ikilinganishwa na wanaume ambao hawana tatizo hili.

3.Kuathirika kisaikolojia (kuona aibu, kutojiamini, kujihisi tofauti na wanaume wenzake). Hali hii inaweza hata kumfanya mtu kuishi maisha ya huzuni au kushindwa kujumuika na watu katika shughuli mbalimbali kama michezo na nk

0 comments:

Post a Comment